
NCHI ya Tanzania, ndani ya miaka 51
ya uhuru wake, imekuwa na matukio ya kusisimua yanayohusu soka yake
kama vile Cosmopolitan ya jijini Dar es Salaam kuwa klabu ya kwanza ya
Tanzania kuiwakilisha nchi yetu kwenye mashindano ya vilabu ya bara hili
mwaka 1967.
Kuna kipigo cha Yanga kwa Simba
(wakati huo Sunderland) cha mabao 5-0 mwaka 1969, Yanga kutupwa nje ya
mashindano ya klabu bingwa Afrika na Asante Kotoko ya Ghana kwa kura ya
shilingi jijini Dar es Salaam mwaka 1969 na Simba kubeba ubingwa wa
kwanza wa vilabu vya Afrika Mashariki katika mashindano ya kwanza kabisa
mwaka 1974 jijini Dar es Salaam.

Kuna tukio la Mseto ya Morogoro
kubeba ubingwa wa Tanzania ikiwa klabu ya kwanza kutoka Dar es Salaam
kufanya hivyo mwaka 1975 baada ya kuilaza kwenye fainali Nyota ya Mtwara
kwa mabao 3-1. Hiyo ilikuwa fainali isiyo ya Yanga na Simba kwani
enzi hizo za bingwa wetu kupatikana kwa mtoano, fainali zilikuwa baina
ya Yanga na Simba tu, ukiondoa mwaka 1973 zilipokutana kwenye nusu
fainali, Simba kuilaza Yanga 1-0, kucheza fainali na Lake Stars ya
Kigoma, kushinda 2-0 na kubeba ubingwa.
Lipo tukio la Simba kufika hatua ya
nusu fainali ya klabu bingwa ya Afrika mwaka 1974, mwaka ambao ulikuwa
wa mechi ya Yanga na Simba inayoongoza kwa msisimko hadi sasa ya
Nyamagana Mwanza ambapo kwenye dakika ya 87, Yanga ilisawazisha bao la
Simba la dakika ya 16 na kupata la ushindi kwenye dakika 30 za nyongeza.
Bao la Simba lilifungwa na Adam Sabu aliyeingia badala ya Saad Ali
aliyeumia vibaya. Bao la kusawazisha lilifungwa na Gibson Sembuli na la
ushindi Sunday Manara.
Kuna lile la Yanga kufukuza
wachezaji karibu wote wa kikosi cha kwanza mwaka 1976 na kupigwa 6-0 na
Simba mwaka mmoja baadaye wakiwa wameshajisuka vya kutosha.
Tukio kubwa kuliko yote ni lile la
timu yetu ya Taifa kucheza fainali za mataifa ya Afrika mwaka 1980
nchini Nigeria, tulipofungwa 3-1na Nigeria, 2-1 na Misri na kumaliza kwa
sare ya 1-1 na Ivory Coast. Tuna pointi moja ya mashindano hayo huku
kukiwa na timu miaka hii zinazomaliza bila pointi!

Tukio la kushangaza kuliko yote ni la mwaka 1979 ambapo Simba
ililala hapa 0-4 kwa Mufurira
Wanderers ya Zambia kwenye mashindano ya ubingwa wa Afrika lakini
ugenini wenyeji Mufurira Wanderers walilala 0-5 kwa Simba. Tukio hili
lilikuwa na maajabu mengi ambapo tumechagua matano kulingana na idadi ya
magoli waliyofunga Simba ugenini na kuvuka hadi raundi iliyofuata.
Maajabu hayo ni:-
- Goli la kwanza- Maajabu ni kwamba si rahisi sana kwa timu ya Afrika kulala 4-0 nyumbani na kwenda kushinda ugenini 5-0.
- Goli la pili- mabao matano ya Simba yalifungwa na wachezaji wawili tu, Thuwen Ally matatu na George “Best” Kulagwa mawili.
- Goli la tatu- Mchezaji Willy Mwaijibe, ambaye hakuwa akicheza kwa muda mrefu alicheza vizuri mno mechi hiyo kama kuaga kwani baada ya hapo hakucheza tena mpaka alipofariki dunia mwaka 1991.
- Goli la nne- Kocha wa Simba aliyefanikisha ushindi huo ni mpenzi mkubwa na mwanachama mtiifu wa Yanga, Joel Nkaya Bendera.
- Goli la tano- Rais wa Zambia wa wakati huo, Kenneth Kaunda alikuwepo uwanjani akishuhudia vijana wake wakiadhirika.
Baadaye, Simba ikapambana na Racca
Rovers ya Nigeria na kutupwa nje ya mashindano kwa jumla ya mabao 2-0
baadaya ya kufungwa 2-0 kwenye pambano la ugenini lililofuatia lile la
suluhu la Dar es Salaam. Kwenye pambano la hapa, beki chipukizi wa
Simba, Hussein Tindwa, alianguka uwanjani na kufariki dunia kabla
hajafikishwa hospitalini Muhimbili kwa tatizo la kubana pumzi lililokuwa
la kawaida kwa mchezaji huyo kwa waliomfahamu.
Mwaka 1979 Simba wanafanya maajabu
nchini Zambia kwa kupindua kipigo cha 4-0 nyumbani kwa kipigo cha 5-0
nchini Zambia na halafu mwaka huo huo timu yetu ya Taifa, baada ya
ushindi wa nyumbani wa bao 1-0 la Mohammed “Adolph” Rishard, tunapata
sare nchini Zambia ya 1-1 kwa bao la kusawazisha la Peter Tino, mbele ya
Rais Kaunda tena, na kukata tiketi ya fainali ya mataifa (huru) ya
Afrika nchini Nigeria.
Hiyo ndiyo soka ya ukweli ya miaka
hiyo iliyojaa kila aina ya weledi.Inaleta raha sana kuikumbuka soka
hiyo ikiwa ni ishara isiyo na utata ya uongozi bora wa miaka hiyo wa
nyanja na ngazi tofauti. Riadha, masumbwi, netiboli na michezo ya mtu
mmoja mmoja vyote vilikuwa juu kipindi hicho, ikithibitishwa na medali
pamoja na makombe tuliyokuwa tunapata
No comments:
Post a Comment